Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ameziagiza mamlaka za ulinzi na usalama nchini humo
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ameziagiza mamlaka za ulinzi na usalama
nchini humo kuhakikisha shughuli ya kujiandikisha kwenye daftari la
wapiga kura na upigaji kura ya Katiba Inayopendekezwa unafanyika kwa
amani na wasioitakia mema nchi wasibadilishe matukio hayo kuwa fujo na
kuingiza nchi kwenye vurugu. Rais Kikwete amesema, kazi ya kuboresha
daftari la wapiga kura, imeanzia Njombe na itaendelea mikoa mingine na
kuwataka viongozi hao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi na
kukumbusha maana ya kuwa na kitambulisho cha kura ambacho kitamwezesha
kupiga kura ya maoni na katika uchaguzi mkuu mwaka huu. Rais wa Tanzania
amezungumzia tena suala la mauaji ya albino, usafirishaji wa madawa ya
kulevya na kubainisha kwamba, ni jambo la aibu, kijinga na fedheha kubwa
kwa mtu mzima na akili zake kuamini kwamba, akipata kidole cha albino
mambo yake yatamnyookea na kupata mafanikio ya maisha. Rais Kikwete
amezitaka kamati za ulinzi na usalama za Tanzania zikae na kuona namna
zitavyokabiliana na suala hilo. Wakati huo huo, utata umegubika
uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi Tanzania baada ya Serikali kutaka
kuwasilisha ‘kinyemela’ muswada wa uanzishwaji wa mahakama hiyo, kwenye
Mkutano huu wa 19 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma bila kuupitisha
kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kama
utaratibu unavyotaka.
0 comments:
Post a Comment