Mapigano makali yameanza tena kati ya majeshi ya serikali ya Sudan Kusini na waasi wa nchi hiyo, ikiwa yamepita chini ya masaa 48 tokea yalipofanyika mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili.
Msemaji wa kundi la waasi Lul Ruai Koang amedai kwamba, majeshi ya serikali ya Sudan Kusini yameanzisha vita hivyo kwa kushambulia maeneo kadhaa katika majimbo ya Unity na Upper Nile. Koang ameongeza kuwa, lengo la majeshi ya serikali ya Juba kufanya mashambulio hayo, ni kutaka kuvidhibiti visima vya mafuta vilivyoko katika maeneo hayo, ambavyo vinadhibitiwa na waasi.
Siku chache zilizopita, ilifanyika duru ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi wanaongozwa na Riek Machar, makamu wa zamani wa rais, chini ya upatanishi wa Jumuiya ya Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD. Hivi karibuni, mwakilishi wa IGAD alitangaza kwamba, pande hizo mbili zimekubaliana kuheshimu makubaliano ya kukomesha vita vilivyodumu kwa miezi kadhaa nchini humo.
0 comments:
Post a Comment