Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
amesisitiza juu ya udharura wa kushirikiana nchi za eneo la Mashariki ya
Kati ili kuyapatia ufumbuzi matatizo ya mazingira ya eneo hili. Rais
Hassan Rouhani amesisitiza juu ya udharura wa kushirikiana nchi za eneo
ili kutatua matatizo ya mazingira na kusisitiza kuwa mazingira na
usalama wa watu kamwe haviwezi kukabiliwa na hatari kutokana na vikwazo
vilivyo kinyume cha sheria, iwapo kutakuweko na mtazamo wa pamoja wa
kibinadamu na kulifanya suala la usalama kuwa mhimili mkuu. Rais wa
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo katika hotuba aliyoitoa jana
mjini New York kwenye kikao cha wakuu wa nchi kuhusu mabadiliko ya tabia
nchi.
Rais Hassan Rouhani amekitaja kikao
hicho cha wakuu wa nchi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kuwa ni fursa
nzuri ya kuzungumzia mabadiliko ya tabia nchi kama moja ya changamoto
muhimu za karne ya 21 na kueleza kuwa, ongezeko la joto duniani na
athari zake za kupungua mvua katika eneo la Mashariki ya Kati, ukame wa
mfululizo na kupungua maji, yamezidisha umaskini na kupelekea uwezekano
wa kuibuka machafuko na mivutano ya mpakani; hata hivyo akasema kuwa kwa
bahati mbaya kuendelea mizozo ya kisiasa na vita katika nchi jirani pia
kumekuwa kikwazo cha kufikiwa makubaliano ya kivitendo na ya kudumu kwa
ajili ya kutatua matatizo ya mazingira katika eneo hili. Dakta Hassan
Rouhani amesema pia kwamba kuibuliwa vizingiti vya aina yoyote katika
njia ya ushirikiano wa nchi za ulimwengu katika kutatua matatizo ya
mazingira kutakuwa kwa madhara ya jamii ya kimataifa.
Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran jana pia alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Recep
Tayyep Erdogan wa Uturuki pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa huko New York. Katika mazungumzo hayo Marais wa Iran na
Uturuki walishauriana juu ya njia ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi
mbili hizo. Mbali na Rais wa Uturuki, Rais Hassan Rouhani alikuwa na
mazungumzo pia na Rais wa Ufaransa, Venezuela na viongozi wengine
kadhaa.
0 comments:
Post a Comment