Jumatatu ya tarehe 22 Septemba
wawakilishi wa serikali na wapinzani wa Sudan Kusini walianza duru mpya
ya mazungumzo ya amani katika viunga vya mji mkuu wa Ethiopia Addis
Abab. Hii ni mara ya kwanza kwa pande mbili hizo hasimu za Sudan Kusini
kukutana tangu yalipotiwa saini makubaliano ya nne ya usitishaji vita
mwishoni mwa mwezi uliopita. Jumuiya ya Ustawi ya nchi za mashariki mwa
Afrika IGAD ndiyo msimamizi wa mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini
ambayo tangu yalipoanza yamekuwa na mwendo wa kinyonga. Mada kuu katika
duru hii mpya ya mazungumzo ni kuundwa serikali ya mpito na ya umoja wa
kitaifa. Suala la kuchaguliwa Rais na Waziri Mkuu ni ajenda nyingine
muhimu katika duru hii ya mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini huko
Ethiopia.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa,
kuchaguliwa Rais na kuainishwa nguvu na mamlaka ya Waziri Mkuu kitakuwa
kibarua kigumu mno hasa kwa kutilia maanani historia ya vita vya kuwania
madaraka kati ya Rais wa sasa Salva Kiir na Riek Machar aliyekuwa
Makamu wa Rais na ambaye kwa sasa ndiye kiongozi mkuu wa upinzani. Taban
Deng Gai, mkuu wa timu ya wapinzani katika mazungumzo na serikali ya
Juba ameituhumu serikali kwamba, imekiuka makubaliano ya usitishaji
vita. Kwa upande wake serikali ya Sudan Kusini nayo inamtuhumu kiongozi
wa upinzani Riek Machar kwamba, amekiuka vipengee vya hati ya
makubaliano. Nchi changa zaidi barani Afrika ya Sudan Kusini ilitumbukia
katika dimbwi la machafuko kuanzia Desemba mwaka jana baada ya kuzuka
mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na wale watiifu kwa aliyekuwa
Makamu wa Rais Riek Machar. Mapigano hayo yalienea kwa kasi kubwa na
kugubika nchi yote. Hata kutiwa saini makubaliano ya usitishaji vita
hakujawa dawa mujarabu, kwani mara kadhaa hati ya makubaliano hayo
imekiukwa; na hivyo kushuhudiwa mapigano yakiendelea. Ni kwa kuzingatia
kuweko kizungumkuti hicho, ndiyo maana hata suala la uundwaji wa
serikali ya umoja wa kitaifa nalo limeakhirishwa. Wapembuzi wa masuala
ya kisiasa wanaamini kuwa, vita vya madaraka kati ya Salva Kiir na Riek
Machar ndicho chanzo cha kuibuka machafuko katika nchi hiyo changa
ambayo ilitangaza rasmi kujitenda na Sudan Kuu Julai 2011. Mbali na
machafuko, kwa sasa Sudan Kusini kama wanavyosema wataalamu wa Umoja wa
Mataifa inakabiliwa pia na upungufu mkubwa wa chakula. Wataalamu wa
Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, hali ya upungufu wa chakula
inayokabiliwa nayo Sudan Kusini ni mbaya mno ikilinganishwa na maeneo
mengine duniani yanayotaabika na hali hiyo. Fauka ya hayo, mashirika ya
utoaji misaada yametoa indhari kuhusiana na nchi hiyo kukumbwa na ukame.
Ni kwa kuzingatia matatizo mbalimbali yanayoikabili Sudan Kusini ndio
maana wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuna haja kwa mgogoro wa
kisiasa wa nchi hiyo kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekano, ili kwa njia
hiyo kuandaliwe uwanja wa kuyashughulia matatizo mengine yanayoikabili
nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment