Sunday, 28 September 2014

Mtazamo wa Rais Hassan Rouhani wa Iran  juu ya namna ya kutokomeza ugaidi
 Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye ametoa pandekezo la kuasisiwa muungano wa kimataifa dhidi ya ghasia na uchupaji mipaka duniani, ameeleza kuwa kupambana kimaonyesho na ugaidi hakuwezi kuifanya dunia kuwa bara ya amani na utulivu. Dakta Rouhani ambaye jana alasiri alikuwa akizungumza na wawakilishi wa vyombo vya habari vya kimataifa huko New York, Marekani alisisitiza kuwa, ugaidi una vyanzo mbalimbali na kwamba sera sahihi za kupambana na hatari hiyo kubwa inayotishia ulimwengu ni kutokomeza sababu za kiaidiolojia na kibinadamu na vyanzo vya kifedha na kisilaha vya ugaidi. Rais Hassan Rouhani amesema kuwa nchi zinatumika kusafirisha magaidi hazipasi kuyaruhusu makundi ya kigaidi kuwashawishi na kusajili watu kutoka katika pembe mbalimbali ili kujiunga na makundi hayo.
Tishio la ugaidi ni changamoto kubwa inayozikabili nchi mbalimbali duniani. Sehemu kubwa ya tishio hilo inasababishwa na siasa za undumakuwili za wale wanaodai kuwa wanaendesha mapambano dhidi ya ugaidi kwa ajili ya kutokomeza tatizo hilo kubwa katika karne ya sasa. Kuanza mgogoro huko Syria na kushtadi harakati za magaidi katika eneo la Mashariki ya Kati, yote hayo yana uhusiano maalumu na siasa na undumakuwli na zinazokinzana za Magharibi katika kupambana na ugaidi. Baadhi ya nchi za eneo hili zikiwemo Uturuki, Jordan, Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Magharibi hususan Marekani tangu mwaka 2011 ziandaa mazingira ya kuingia magaidi katika eneo hili. Katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu iliyopita magaidi waliweza kuingia kwa urahisi huko Uturuki wakitokea katika maeneo mbalimbali ya dunia na kisha wakaingizwa nchini Syria. Sambamba na hatua hiyo, magaidi hao walipatiwa silaha za aina mbalimbali za Marekani na Israel kupitia njia tafauti.
Kwa jumla miamala ya harakati ya Kiarabu-Magharibi katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu iliyopita imepelekea kuimarika ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na kutia nguvu sera za kutumia ugaidi kwa ajili ya malengo yao. Siasa hizo hatimaye zimezidisha hatari ya ugaidi na sasa ugaidi wa kundi la Daesh walioulea na kuupalilia wao wenyewe umewageukia waanzilishi wake hususan Marekani na Saudi Arabia.
Utoro huo wa kundi la kigaidi la Daesh umekuwa kisingizio cha Marekani kuianzisha eti muungano wa kupambana na ugaidi ambao umeundwa bila ya kuzingatia sheria za kimataifa hususan zile za Umoja wa Mataifa. Muungano huo sasa umeanzisha mshambulizi dhidi ya kundi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria.
Uzoefu wa miaka 13 ya mashambulizi ya nchi za Magharibi huko Pakistan na Afghanistan umeonesha kwamba, mashambulizi ya anga si tu kwamba hayakuweza kuangamiza ugaidi, bali yameuimarisha zaidi. Kwa msingi huo inabainika kuwa, miongoni mwa siasa sahihi za kutokomeza ugaidi ni pamoja na kukomesha misaada ya kifedha, kijeshi na kisiasa kwa makundi ya kigaidi, kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kuheshimu mamlaka ya kujitawala ya nchi mbalimbali zinazosumbuliwa na ugaidi.
Kufanyiwa kazi pendekezo la Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kuundwa muungano wa kimataifa wa kukabiliana na machafuko na misimamo mikali kote duniani ni stratijia muhimu katika njia sahihi ya kupambana na ugaidi na kunaweza kurejesha amani na utulivu duniani. Rais Hassan Rouhani anasisitiza kuwa maulamaa, wasomi, wanafikra na waandishi ndio wenye jukumu kubwa zaidi la kupambana na ugaidi kwa sababu harakati za kigaidi hazina mfungamano wowote na dini za mbinguni hususan Uislamu.
Kwa msingi huo inaonekana wazi kuwa, mchezo wa kuigiza wa kihollywoodi na kutumia nguvu za kijeshi pekee eti kwa ajili ya kutokomeza ugaidi hauwezi kung'oa mzizi wa uovu huo.

0 comments:

Post a Comment

Translate

facebook

TANGAZA HAPA

KWA HABARI MAKINI

Napokea maoni muhimu kwa pale unapoona apakustahili kuwepo kwenye blogg yetu makini yenye lengo la kukuunganisha pamoja na kuelimishana kwa yale mazuri yote piga simu kwa chochote muhimu namba zipo apo juu

NEWS