Duru za habari nchini Kenya zimeripoti taarifa ya kutekwa nyara kiongozi
mmoja wa serikali ya nchi hiyo na kundi la kigaidi na kitakfiri la
ash-Shabab la nchini Somalia. Mukhtar Maalim Adan, ambaye ni afisa
utawala katika mji wa Mandera nchini Kenya, ametekwa nyara na kundi hilo
ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara nchini humo.
Maafisa wa polisi wamesema kuwa, Mukhtar ametekwa nyara alipokuwa
safarini kutoka mjini Mandera kuelekea moja ya miji ya nchi hiyo ya
Afrika Mashariki ambapo alivamiwa na wanachama wa kundi hilo na kisha
kuchukuliwa kwa gari lake na kupelekwa kusikojulikana. Hadi sasa polisi
bado haijafanikiwa kunasa gari ya Mukhtar Adan na ingali inaendelea na
uchunguzi kuwabaini wahusika wa tukio hilo. Hata hivyo polisi ya Kenya
ina wasi wasi kwamba huwenda kiongozi huyo wa serikali akawa amepelekwa
Somalia na kundi hilo la kigaidi. Mji wa Mandera uko katika mpaka wa
pamoja wa Kenya na Somalia ambapo unatajwa kuwa njia mojawapo muhimu
inayotumiwa na wanachama wa ash-Shabab kuingilia nchini Kenya na
kutekeleza uhalifu wao. Licha ya kwamba hadi sasa hakuna kundi lolote
lililotangaza kuhusika na tukio hilo la utekaji nyara, lakini kidole cha
lawama kimeelekezwa kwa kundi hilo ambalo wiki kadhaa zilizopita,
lilitekeleza hujuma kali dhidi ya Chuo Kikuu cha mji wa Garissa
kaskazini mashariki mwa Kenya na kuua watu 150 wengi wao wakiwa ni
wanafunzi.
Thursday, 23 April 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment