Rais Jakaya Kikwete amezindua chapisho la tatu la taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi litokanalo na sensa ya mwaka 2012, huku akieleza kuridhishwa na hatua ambayo Tanzania imefikia, hususan kwenye utekelezaji wa malengo ya milenia na dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.
Taarifa za chapisho hili, zinaweka wazi uwezekano wa Tanzania kufikia malengo hayo kwa wakati, kwa kuwa tayari imepiga hatua kubwa kwenye maeneo muhimu yanayoainishwa kwenye MDG na Vision 2025.
Miongoni mwa maeneo yanayotajwa na Rais, ni kupungua kwa vifo vya akina mama na watoto pamoja na kupanda kwa hali ya uchumi inayojiainisha kwenye uboreshaji wa makazi binafsi, umiliki wa vifaa na kupanda kwa kipato, huku akiwataka watendaji wa ngazi zote kutumia vema taarifa hiyo.
Hata hivyo changamoto katika kufikia hatua hizi za kimaendeleo inabaki kuwa ni ongezeko la idadi ya watu, ambapo taarifa ya mwisho iliyotolewa mwaka huu inaonyesha idadi hiyo kufikia milioni 44.9, na ikitarajiwa kufikia milioni 63, ifikapo mwaka 2025, na milioni 125 ifikapo mwaka 2050.
Awali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema machapisho ambayo tayari yamekwishatoka hadi sasa, huku mengine 11 yakitarajiwa kutolewa kabla ya mwezi september mwaka huu.
Taarifa ya matokeo ya chapisho hili iliwasilishwa na ofisi ya taifa ya takwimu, na hii ni sehemu tu ya taarifa hiyo.
Taarifa iliyotolewa imegusia maeneo muhimu ya sensa za makazi ambayo imeonesha kupanda kwa idadi ya watanzania wenye vyeti vya kuzaliwa kwa asilimia 15, ongezeko la idadi wanaoandikishwa shule kwa asilimia 77, kupungua kwa kiwango cha uzazi na kuongezeka kwa urefu wa maisha ya mtanzania ambapo kwa sasa ni miaka 61 toka miaka 50 ya mwaka 1988.
Huu ni uzinduzi wa chapisho la tatu la taarifa za msingi za kidemografia, kijamii, na kiuchumi linalotokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012,pamoja na matumizi ya tovuti katika kupata taarifa mbalimbali za sensa ya watu na makazi.
MWISHO.
Napitia Chapisho la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi nchini ambalo limetolewa jana ikiwa ni sehemu ya Sensa ya mwaka 2012. Hii ni moja ya tafiti muhimu sana katika kupanga mipango ya maendeleo na pia katika kujadili mustakabali wa nchi yetu. Baadhi ya takwimu katika utafiti huu ni:
1. Idadi ya watu Tanzania inakua kwa asilimia 2.7 kwa mwaka. Kwa kiwango hicho idadi ya watu nchini itakuwa mara mbili ya sasa katika kipindi cha miaka 26 ijayo na itafikia watu milioni 90.
2. Asilimia 44 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 15, asilimia 4 wana miaka 65 kwenda juu na kwa watoto wenye miaka 10 kwenda chini wavulana ni wengi kuliko wasichana.
3. Ni asilimia 15 tu ya Watanzania wana vyeti vya kuzaliwa.
4. Kwa wastani asilimia 1% ya kaya zote nchini imeripoti kuwa na walau mtu mmoja aishiye nje ya Tanzania. Mwaka 2012 Tanzania ilikuwa na jumla ya watu 421,456 waishio na kufanya kazi nje ya Tanzania.
5. Kiwango cha wanaojua kusoma na kuandika ni asilimia 72 toka asilimia 63 mwaka 2002. (Asilimia 89 mijini, vijijini asilimia 64; kati ya mkoa na mkoa: Dar es Salaam asilimia 96, Tabora asilimia 59)
6. Asilimia 48 ya kaya zote zinaishi katika nyumba zao wenyewe. Asilimia 31 hawana haki ya kisheria kwenye maeneo waliyojenga nyumba zao.
7. Mali ambazo kaya zinamiliki kwa wingi: nyumba (75%), jembe la mkono (74%), shamba/ardhi (70%), simu za mkononi (64%). Wanaume wanamiliki mali nyingi zaidi kuliko wanawake.
8. Umri wa wastani wa Mtanzania ni miaka 17.1.
9. Vyanzo vya nishati ya kupikia katika kaya mbalimbali ni: nishati itokanayo na miti inatumiwa na asilimia 94 ya kaya zote (68.5% wanatumia kuni, 25.7% wanatumia mkaa). Asilimia 58 ya kaya zinatumia mafuta ya taa kama nishati ya kujipatia mwanga.
10. Wastani wa idadi ya watu kwa kila kaya ni watu 4.7. Asilimia 33.4 ya kaya zote nchini zinaongozwa na wanawake. Kaya zinazoongozwa na wanawake zina idadi kubwa zaidi ya watu (watu 7.4 kwa kaya) kuliko kaya zinazoongozwa na wanaume (watu 3.5).
0 comments:
Post a Comment